May 24, 2018





Kampuni ya SportPesa Limited leo siku Alhamisi tarehe 24 Mei imekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 100 kwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba SC.


Hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi za SportPesa ambao ni wadhamini wakuu wa Wekundu hao wa msimbazi zilizopo maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam, ilihudhuriwa na viongozi wa pande zote mbili kutoka SportPesa ni Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Pavel Slavkov, Mkurugenzi wa Utwala na Utekelezaji Tarimba Abbas na Mkuu wa kitengo cha Operesheni Luca Neghesti kutoka Simba ni Kaimu Makamu wa Raisi Ndugu Iddi Kajuna, Katibu Mkuu Hamisi Kissiwa.

Msemaji mkuu wa kampuni Haji Manara pamoja na Mjumbe wa kamati ya Usajili Said Tulliy sambamba na wachezaji wote wa kikosi cha Simba wakiongozwa na nahodha John Bocco.


Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Ndugu Tarimba Abbas alianza kwa kuwapongeza wachezaji na viongozi wa Simba kwa kutwaa ubingwa.


“Awali ya yote nianze kwa kuwapongeza viongozi na wachezaji wa Simba SC kwani mmewapa heshima kubwa wana msimbazi kote nchini na kubwa zaidi ni heshima mliyotupa sisi kama wadhamini wenu wakuu.


Ndugu Abbas aliendelea kwa kufafanua kuhusu kiasi hicho cha pesa ambacho SportPesa imekabidhi kwa Simba kwa kusema;

“Simba imeitendea haki nembo yetu ya SportPesa na kampuni inaamini kuwa kwa SportPesa kuwa wadhamini wakuu imekuwa ni moja ya chachu iliyosababisha Simba Sports Club kuchukua ubingwa huu”

“Tunachokifanya leo ni kutimiza moja ya ahadi tuliyotoa wakati tunasaini mkataba mwezi Mei mwaka jana kuwa tutatoa bonasi ya Shilingi Milioni 100 endapo mojawapo ya timu tunazozidhamini itachukua ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo bila shaka timu ni Simba SC”, alihitimisha.

Akiongea kwa niaba ya Simba SC, Makamu wa Rais wa mabingwa hao mara 19 wa Tanzania Bara Ndugu Salim Abdallah alianza kwa kuishukuru kampuni ya SportPesa kwa kuwa nao bega kwa bega

“Moja ya jambo ambalo Simba inajivunia msimu huu ni kuwa na mdhamini kama SportPesa ambaye mbali na udhamini, pia tumekuwa tukishirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuongozi.

“Tulifanya maandalizi mazuri msimu huu kuanzia kwenye ngazi ya uongozi hadi benchi la ufundi na ndio maana sio jambo la ajabu Simba kuwa bingwa kwani tulishaandaa mikakati kwa kushirikiana na wadhamini wetu, SportPesa.


“Niwashukuru SportPesa kwa moyo wao wa kuleta mabadiliko ya soka nchini ambayo sisi kama Simba SC tumeyaona kwa upande wetu na tutaendelea kutoa ushrikiano katika miaka mingine minne iliyosalia kwenye mkataba wetu”, alisisitiza Kajuna.


Simba SC ni miongoni mwa timu nne kutoka Tanzania zitakazoshiriki kwenye michuano ya SportPesa Super Cup itakayofanyika nchini Kenya kuanza Juni 3-10 ikishirikisha timu nane kutoka nchi za Tanzania na Kenya.


Timu nyingine ni pamoja na Yanga, Singinda United na JKU kutoka Tanzania sambamba na Gor Mahia, AFC Leopards, Kakamega Home Boys sambamba na Kariobangi Sharks kutoka Kenya ambapo mbali na kujizolea kitita cha Dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo ataenda nchini Uingereza kucheza dhidi ya Everton FC kwenye dimba la Goodison Park.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic